HISTORIA YA DCU

Historia inaonyesha kuwa udhibiti na usimamizi wa ujenzi ni suala ambalo lilipewa umuhimu mkubwa sana Zanzibar. Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali iliwekwa ili kusimamia masuala ya ujenzi na matumizi bora ya ardhi kwa ujumla. Tangu wakati wa ukoloni zilikuwepo sheria nyingi na Kanuni zilizohusiana na masuala ya ujenzi hususan kwa maeneo ya Ng\'ambo ambako ndiko kulikokuwa kunaendelezwa zaidi. Sheria kuu tatu ambazo ndizo zilizokuwa zikitoa miongozo ya ujenzi ni Sheria ya Miji (Cap 79 ya mwaka,1929); Sheria ya Miji Midogo (Cap 80 ya mwaka,1944) na Sheria ya mipango Miji na Vijiji (Cap 85 ya mwaka1955). Utekelezaji wa Sheria hizo ulitegemea sana mfumo wa Serikali za mitaa uliokuwepo wakati huo.

Kimsingi mfumo wote wa utawala Zanzibar ulibadilika baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Mwaka 1968, Serikali ilifuta mfumo wa Serikali za mitaa uliokuwepo. Katika kuweka mfumo mzuri, Serikali ya Mapinduzi ilianza kuzibadilisha baadhi ya sheria, kuzifuta zilizokuwa hazistahiki na kutengeneza sheria mpya pamoja na kufutwa kwa baadhi ya taasisi. Hatua hii ilileta changamoto katika suala la usimamizi na udhibiti ujenzi Zanzibar hususan katika maeneo ya miji. Kufutwa kwa taasisi hizo kulipelekea sheria na kanuni zilizokuwepo chini ya sheria hizo, yaani Cap 79,80 &85, kubaki bila kuwa na vyombo madhubuti vya usimamizi. Hatua hiyo ilipelekea Idara ya Ujenzi iliyokuwa chini ya Wizara ya Ufundi, Njia na Simu kuwa ndio msimamizi wa utoajii wa vibali vya ujenzi.

Changamoto zaidi zilitokea mwaka 1986, baada ya kuanzishwa kwa sheria Nambari 3 ya Mamlaka za Serikali za Wilaya na Miji, (Local GovernmentDistrict and Urban Authorities- Act, No 3 of 1986). Sheria hiyo mpya ilizifuta sheria za zamani zinazohusu Usimamizi wa Miji Midogo na Kanuni za Ujenzi (Township Decre Cap 80 & Building Regulation Cap.79). Kwa kiwango kikubwa sheria hizo mbili hususan Cap.79 ndizo zilizokuwa zikitoa muongozo wa shughuli zote za ujenzi nchini.

Sheria ya mwaka 1929 (Cap 79), ndiyo iliunda Joint Building Authority -JBA chombo ambacho kikisimamia shughuli zote za utoaji wa vibali vya ujenzi wa aina zote Zanzibar, Kanuni za sheria hizo pia ziliweka adhabu kwa wale wote waliokuwa wakikiuka taratibu za ujenzi. Aidha, Sheria ya Mipango Miji na Vijiji sura ya 85 ya mwaka 1955 pamoja na Kanuni hizo za miji na ujenzi ndizo zilizokua msingi wa usimamizi na udhibiti wa matumizi bora ya ardhi nchini.

Kwa maoni ya wengi sheria iliyopaswa kufutwa ni Cap. 80 na baadhi ya vifungu vya Cap.79. Sheria mpya ya Mamlaka za Wilaya na Miji ya mwaka 1986 ilikuwa ni mbadala wa Cap.80 na sio Cap79. Kwa mantiki hiyo kuanzia mwaka 1986, Zanzibar haikuwa na muongozo imara wa ujenzi unaojulikana kisheria ijapokuwa Sheria Nambari.3 ya mwaka 1986 ilijaribu kubeba baadhi ya vifungu vya Cap 79 ya mwaka 1929. Hali hiyo ndio ikawa chanzo cha matatizo ya ujenzi holela katika miji na vijiji kwa vile hakukuwa na chombo kilichokuwepo kisheria kusimamia na kudhibiti ujenzi. Mbali ya changamoto za kisheria suala la ujenzi holela pia lilichangiwa na, ukosefu wa makaazi bora, ongezeko la watu, na kutotekelezwa kwa Mipango ya Miji (Master Plans). Mwaka 1986, zilitungwa sheria mbili mpya kuhusu Mabaraza ya Manispaa na Miji (Municipal na Town Councils). Sheria hizi zikafuta kabisa ile dhana ya Urban Authority iliyokuwepo kwenye Sheria Namba 3 ya mwaka, 1986. Kufuatia changamoto hizo msingi wa kisheria wa masuala ya ujenzi ukazidi kupotea. Kwa kuziba pengo hilo, mwaka 1998 Serikali ilianzisha chombo cha muda cha udhibiti ujenzi Kilichoitwa Urban Development Control Authoritiy- UDCA ikiwa ni kama mbadala wa JBA. Aidha, Chombo hiki kipya kilianzishwa kwa kutumia kifungu cha sheria ya Mipango Miji na Vijiji ( Cap 856 (1955). Kuanzia mwaka 1998, suala la udhibiti ujenzi likawa linasimamiwa na UDCA. Hata hivyo, UDCA nayo ilikabiliwa na changamoto mbalimbali na haikuweza kufanya kazi zake kama ilivyotarajiwa. Aidha, UDCA ilikuwa inafanya kazi katika maeneo ya miji tu hususan Manispa ya mji wa Zanzibar na Mji wa Chake Chake.

Sheria ya Mamlaka za Wilaya na Miji ya mwaka 1986 ilipofutwa na kuanzishwa kwa Sheria Nambari 3 na 4 za mwaka 1995 za kuanzishwa kwa Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya bado hazikuzingatia urejeshwaji wa masuala ya udhibiti na usimamizi wa ujenzi katika mamlaka hizo. Mapitio ya sheria hizi mwaka 2014 hazikuweza kuziba pengo lililowachwa na sheria ya mwaka 1926, Cap 79.Kutokana na changamoto hizo zilizotokea katika miaka hiyo ya 1968 -2015, na ili kutilia nguvu utekelezaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Mji na Vijiji kwa Unguja na Pemba (NSDS, Master Plans & Local Area Plans), Serikali iliamua kuanzisha chombo kipya cha Usimamimizi na Udhibiti Ujenzi ( Development Control Unit - DCU ).


DHAMIRA YA DCU



Ni Kuongeza udhibiti wa maendeleo kupitia ufanisi, mfumo wa uwazi na shirikishi wa matumizi endelevu ya ardhi na maendeleo hapa Zanzibar

Copyright ©2024 DCU